Leviticus 1

Sadaka Ya Kuteketezwa

1 a Bwana akamwita Musa na kusema naye kutoka kwenye Hema la Kukutania, akamwambia, 2 b“Sema na Waisraeli na uwaambie, ‘Yeyote miongoni mwenu aletapo sadaka ya mnyama kwa Bwana, alete mnyama kama sadaka yake kutoka kundi lake la ng’ombe au la kondoo na mbuzi.

3 c“ ‘Kama sadaka hiyo ni ya kuteketezwa kutoka kwenye kundi la ng’ombe, atamtoa ng’ombe dume asiye na dosari. Ni lazima amlete kwenye ingilio la Hema la Kukutania ili aweze kukubalika kwa Bwana. 4 dAtaweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka ya kuteketezwa, nayo itakubaliwa kwa niaba yake ili kufanya upatanisho kwa ajili yake. 5 eAtamchinja yule fahali mchanga mbele za Bwana, kisha wana wa Haruni kuhani wataleta damu na kuinyunyiza pande zote za madhabahu yaliyo penye ingilio la Hema la Kukutania. 6 fAtaichuna hiyo sadaka ya kuteketezwa na kuikata vipande vipande. 7 gWana wa Haruni kuhani wataweka moto juu ya madhabahu na kupanga kuni juu ya huo moto. 8 hKisha wana wa Haruni kuhani watapanga vile vipande vya nyama, pamoja na kichwa na mafuta ya huyo mnyama juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu. 9 iAtaziosha sehemu za ndani na miguu yake kwa maji, naye kuhani atavichoma vyote juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, yenye harufu nzuri ya kumpendeza Bwana.

10 j“ ‘Kama sadaka ni ya kuteketezwa kutoka kwenye kundi la kondoo au mbuzi, atamtoa mnyama dume asiye na dosari. 11 kAtamchinjia upande wa kaskazini wa madhabahu mbele za Bwana, nao wana wa Haruni kuhani watanyunyizia damu yake pande zote za madhabahu. 12Atamkata vipande vipande, naye kuhani atavipanga, pamoja na kichwa na mafuta ya mnyama juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu. 13 lAtaosha sehemu za ndani na miguu kwa maji, naye kuhani atavileta vyote na kuvichoma juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Bwana.

14 m“ ‘Kama sadaka ya kuteketezwa inayotolewa kwa Bwana ni ndege, atamtoa hua au kinda la njiwa. 15 nKuhani atamleta kwenye madhabahu, naye atamvunja shingo na kumnyofoa kichwa na kumchoma juu ya madhabahu. Damu yake itachuruzishwa ubavuni mwa madhabahu. 16 oAtaondoa kifuko cha chakula pamoja na uchafu wake na kuvitupa upande wa mashariki wa madhabahu, mahali pale penye majivu. 17 pAtampasua na kumweka wazi katika mabawa yake, lakini asimwachanishe kabisa, kisha kuhani ataichoma juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Bwana.
Copyright information for SwhKC